Utangulizi kwa Kiswahili

 

UTANGULIZI NA HISTORIA YA USHIRIKIANO WA MUDA MREFU KATI YA KIJIJI CHA OLDONYOWAS, JESPER LAND GREGERSEN NA USHIRIKA WA MRADI WA KIJIJI KWA KIJIJI

Mwanzilishi wa mradi wa ushirika wa Kijiji kwa Kijiji anaitwa Jesper Land Gregersen. Aliyepata mafunzo ya utengenezaji zana mbalimbali huko Grundfos, Bjerringbro Denmark miaka ya 1970.  Mara baada ya kumaliza mafunzo alihitaji kusafiri nje ya nchi kitu ambacho kilimpelekea kuja Tanzania chini ya ushirikiano wa kimataifa kufanya kazi za kujitolea.

Kipindi cha miaka ya 1978 hadi 1982 aliajiriwa kama mwalimu wa ufundi katika  mji wa Tanga uliopo katika eneo la ukanda wa Pwani.  Mwaka 1991 hadi 1998 alifanya kazi za kujitolea katika kijiji cha Oldonyowas kilichopo wilaya ya Arusha, ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania.  Wakati huo pia Jesper alipata mafunzo na ujuzi  katika fani ya misitu, awali kazi yake ilikua kuanzisha vitalu vya miche ya misitu – miti, kilimo cha mboga mboga  lakini kazi kubwa ya Jesper ikawa ni kuangalia shida kubwa iliyopo katika kijiji ya upatikanaji wa maji, ambayo ilithibitika kuwa ni vigumu sana kwa wana kijiji kuitatua peke yao bila ya msaada mkubwa wa watu wa nje ya kijiji. 

Kwa sababu hiyo, Jesper kwa ushirikiano mkubwa wa wajumbe wa baraza wa kijiji waliadhimia kuchukua jukumu la kuboresha upatikanaji wa maji kijijini, jitihada ambayo  yeye binafsi ameendelea kuifanyia kazi  kwa ushirikiano wa karibu na wanakijiji, baraza la kijiji na mashirika mbalimbali yanayohusika na maendeleo ya jamii.  Ufadhili wa miradi hii umengwa mkono pamoja na wengineo ni klabu ya Rotary, Grundfos na  mashirika na watu binafsi  mbalimbali.

MRADI WA MAJI SAFI YA KUNYWA

Olodonyowas iko kati ya mwinuko wa mita 1800 pembezoni ya Mlima Meru, ambao ni mlima wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania, na jirani kabisa na mlima maarufu zaidi, Kilimanjaro ambao upo karibia kilomita 80 kwa upande wa mashariki.  Kijiji cha Oldonyowas kinapatikana pembezoni mwa barabara kuu itokayo jiji la Arusha kuelekea Nairobi nchini Kenya.  Arusha ambayo ni jiji kuu katika ukanda huu iko karibia kilomita 35 kutoka Oldonyowas.

Kama ilivyoelezwa hapo awali,  ushirikiano kati ya Oldonyowas na Jesper ulianza mwaka 1991 kwa mradi wa maji ambapo lengo ilikua upatikanaji wa maji safi katika kijiji.  Kama ilivyo kwa maeneo mengi ya volkano kiwango cha madini ya fluorine kiko juu sana ambayo si salama kiafya. Maji ya kunywa haya yako na kiwango hadi 30mg/1 Fluorine wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kiwango kisichozidi 0.5mg/1 Fluorine

Kuwepo kwa kiasi kikubwa zaidi ya kiwango kinachohitajika ya madini hayo kunapelekea  kuharibu madini ya kalisiamu (Calcium) katika mwili na kusababisha ulemavu kwa watu wanaokunywa haya maji.  Hususan baadhi ya wakazi ambao ni wa watu wazima wa hapa Oldonyowas, waweza kuona kabisa athari hiyo kwao inayotokana na kiwango hicho cha juu kilichozidi kwenye maji na uharibifu mkubwa uliowakabili  kwa muda mrefu kupelekea kuwa na hali mbaya ya maisha.

Mradi wa maji safi ya kunywa ulifanikiwa kukamilika mnamo mwaka 1998 baada ya juhudi kubwa ya wanakijiji pamoja na mengine, walishiriki katika kuchimba mitaro kwa ajili ya kupitisha mabomba ya maji, hadi hivi leo kijiji kinaupatikanaji mzuri wa maji safi na salama ya kunywa.  Mradi huu ni moja wapo ya mfano bora wa jinsi gani uchumi wa kijiji na kiwango cha hali ya maisha  ya wanakijiji ilivyoboreka zaidi katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.  Wakati huo huo, wanakijiji wametambua kupitia mradi huu kwamba wao wenyewe wanawajibika  na wanahitajika kuweka jitihada za pamoja katika kuusimamia mfumo huu muhimu kwao wa maji ya kunywa.   Mradi huu wa maji safi ya kunywa ulidhaminiwa na DANIDA.

Wakati huo huo upatikanaji wa maji safi ya kunywa umethibitisha kwamba watoto ambao wamezaliwa na kukua baada ya kukamilika mradi huu wamekua vizuri bila matatizo yeyote na kuwawezesha kucheza mpira wa miguu na kwa ujumla wamekua wachangamfu zaidi kuliko hapo awali.  Hii kwa mfumo wa maji ya kunywa tu.

Mnamo mwaka 2014 mfumo wa maji ya kunywa ulifanyiwa marekebisho makubwa na mhisani ukigharimu kiasi cha 276,000 kr. kutoka kwa Poul Due Jensen’s Fond (Grundfos) Denmark

MRADI WA MAJI KWA MATUMIZI YA NYUMBANI NA UMWAGILIAJI

Baada ya hapo, miradi mingine ya usambazaji maji imekamilika , kama vile mradi wa kurekebisha mfumo wa umwagiliaji, ambao ulikuwa ni lazima kabisa kutekelezwa kwa ajili ya wakulima waliopo kijijini kwa mazao yao, na maji ya kunyweshwa mifugo, kufua nguo na usafi wa mwili kwa ujumla.

Mradi huu pia ulitekelezwa kwa ushirikiano wa Jesper Land Gregersen, Rotary na idadi kubwa ya watu binafsi and mashirika kutoka Denmark na watu wote wa Oldonyowas mnamo mwaka 2017.  Ulikua mradi mkubwa ambao ulichukua miezi 5 kumalizika, kwahiyo sasa Oldonyowas ina miradi miwili inayojitegemea na kufanya kazi vizuri ya kusambaza maji.

Hii mifumo ya maji inatakiwa kuwa kwenye hali nzuri na kufanya kazi vizuri ili kuhakikisha kwamba watu wa Oldonyowas wanapata fursa ya kulima mazao kwenye mashamba yao swala ambalo lina uzito mkubwa katika uchumi wao.

MRADI WA SHULE YA SEKONDARI

Oldonyowas ina jamii inayojituma sana kufanya kazi, pia wana mwamko mkubwa wa maendeleo ya jamii yao.  Uongozi wa Baraza la Kijiji unafanya kazi kila siku kwa bidii ili kuhakikisha kwamba linaboresha  kiwango cha maisha ya kila mmoja katika kijiji chao.  Idadi kubwa  ya watu katika kijiji pia ina mwamko wa kuendeleza jamii yao, ikiwepo kuanzisa mbinu bora za kilimo, kusimamia marekebisho ya  mifumo ya miradi yao mikubwa ya maji na maji ya kunywa, kujenga kituo cha afya na hivi karibuni kuanzisha shule ya sekondari , inayowawezesha watoto kutoka kijijini hapa na maeneo mengine yalipo juu ya kijiji kupata elimu na hivyo kutengeneza msingi wa kuboresha maisha yao na maendeleo ya kijiji.

Kijiji kwa Kijiji inafanya jitihada kubwa na kutatua matatizo mbalimbali  kuwezesha shule hii ya sekondari kuwa kituo bora cha mafunzo ambako mazingira bora ya elimu yanatengenezwa kwa wote wanafunzi na walimu, hii itajenga msingi na kuwavutia walimu wazuri na wanafunzi kusoma hapa ingawa shule iko maeneo mashambani, kuna fursa ya kupata elimu bora ambayo baadae itafaidisha kijiji.

 

Kijiji kwa Kijiji imeanzishwa mwaka 2020 na Jesper Land Gregersen, na haifungamani  na siasa au dini.

 

© 2024 Landsby til Landsby